Thursday, 30 November 2017

WAZIRI MWIJAGE AWAKARIBISHA WATANZANIA KATIKA MAONESHO YA PILI YA BIDHAA ZA VIWANDA VYA TANZANIA

Image result for mwijage akiwa tantrade
Waziri wa Viwanda Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage


Na Thomas Kasumbai Mallya
Waziri wa Viwanda Biashara na Uwekezaji Charles John Mwijage amewakaribisha watanzania wote kuhudhuria na kushiriki katika Maonesho ya pili ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania yanayotarajiwa kuanza tarehe 7-11 Disemba, 2017 katika  Uwanja wa Mwl. J. K. Nyerere Barabara ya Kilwa (Viwanja vya Saba Saba).

Maonesho hayo yanayoandaliwa na Wizara ya  Viwanda Biashara na Uwekezaji kupitia Taasisi yake ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) yanahusisha wamiliki wa Viwanda Vidogo Kabisa, Vidogo,  vya Kati na vikubwa ambapo bidhaa na teknolojia  mbalimbali zinazozalishwa na viwanda hivyo vya kitanzania vikitarajiwa kuoneshwa kwa jamii ya watanzania ambao shauku yao kubwa ni kushuhudia ni kwa namna gani Waziri mwijage anatekeleza agizo la Mheshimiwa Rais Magufuli la Tanzania ya Viwanda.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Waziri Mwijage amesema kuwa kauli mbiu ya maonesho haya ni "Tanzania sasa tunajenga Viwanda" huku akisema kuwa kauli mbiu hii imekuja wakati mwafaka kwani kwa miaka miwili sasa, Tanzania imefanikiwa kujenga viwanda 3306 hivyo hatuna budi kuendelea kujivunia kauli mbiu hii.

Malengo makubwa ya kuandaliwa kwa maonesho haya ni pamoja na kutoa nafasi kwa watanzania kuona taswira halisi ya hali ya viwanda nchini, kuwakutanisha wazalishaji na watoa huduma  mbalimbali za viwanda kwa lengo la kutoa fursa ya kujadili kwa pamoja namna ya kuboresha viwanda vyetu. Aidha, katika maonesho haya wazalishaji watapata fursa ya kutangaza na  kupata masoko ya bidhaa na huduma wanazozalisha. Pia kupitia Maonesho haya, TanTrade itapata fursa ya kuchambua na kutambua bidhaa ambazo tayari zimekidhi viwango vya kutafutiwa masoko ya ndani na nje ya nchi.

Waziri Mwijage amewahamasisha watanzania kuwa na desturi ya kununua na kutumia bidhaa za kitanzania kwani kwa kufanya hivyo tunatengeneza ajira kwa wazalishaji wa bidhaa hizi. Mwijage pia aliwaalika wana taaluma kutembelea  Maonesho haya kwa lengo la kufahamu hatua tuliyofikia katika maendeleo ya viwanda ikiwa ni pamoja na kutumia viwanda vyetu kama "Case study" katika tafiti zao mbalimbali zinazohusu viwanda na biashara badala ya kutumia viwanda vya nje.

"Tanzania kwa mwaka tunanunua kutoka nje jamii ya chakula yenye thamani ya trilioni 3, ambayo ni sawa na asilimia 10 ya bajeti ya nchi hii" .Alisema Mwijage. Tanzania inaingiza bidhaa mbalimbali kutoka nje ya nchi, ambapo bidhaa hizi tuna uwezo wa kuzalisha hapa nchini. Bidhaa tunazoingiza ni pamoja na maziwa, tomato sosi, pilipili, maji ya dripu na nyingine nyingi. Waziri Mwijage amesema Maonesho haya ni muhimu ili watanzania waone umuhimu wa kununua na kutumia bidhaa za kitanzania zinazotengenezwa katika ubora wa hali ya juu.


No comments:

Post a Comment

KASUMBAI