UPASUAJI wa kuzibua mishipa ya moyo bila kufungua kifua kwa kupitia
mshipa wa damu wa mkono kwa wagonjwa 33 uliofanywa na madaktari wa
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) umeibua maajabu mapya kwa
taasisi hiyo inayozidi kujipatia umaarufu mkubwa duniani.
Kwa mara ya kwanza tangu taasisi hiyo imeanza kutoa huduma ya
matibabu ya upasuaji wa moyo bila ya kufungua kifua, hatimaye imeweza
kufanya upasuaji huo wa kuzibua mishipa ya moyo kupitia mshipa wa damu
wa mkono.
Awali wakati huduma hiyo iliponzishwa katika taasisi hiyo ya JKCI,
upasuaji uliokuwa unafanywa kwa wagonjwa waliofika hospitalini hapo
ulikuwa ni ule wa kutumia mishipa ya paja.
Hata hivyo katika tukio la hivi karibuni, madaktari bingwa wa JKCI
kwa kushirikiana na wenzao wa Taasisi ya Kimataifa ya Kiislamu ya
Misaada (IIRO) ya nchini Saudi Arabia walifanya upasuaji huo wa kuzibua
mishipa ya moyo kupitia mshipa wa damu wa mkono kwa kutumia mtambo wa
Cathlab kwa wagonjwa hao 33.
Upasuaji huo wa moyo uliofanyika katika kambi hiyo ya JKCI ambayo
ilianza Novemba 15, mwaka huu hadi jana ni ya upasuaji wa bila kufungua
kifua kwa watu wazima. Pamoja na kuwepo kwa faida mbalimbali kutokana na
upasuaji huo, utafiti wa gazeti hili umebaini kutokea kwa maajabu
mbalimbali kutokana na upasuaji huo.
Ajabu la kwanza la upasuaji huo ni ule ambao sasa utamwezesha mgonjwa
kutoka chumba cha upasuaji akiwa anatembea tofauti na upasuaji wa awali
ambapo mgonjwa hakuweza kutoka kwenye chumba cha upasuaji akiwa
anatembea.
Hiyo ilitokana na upasuaji wa awali kufanyika kwa kutumia mishipa ya
paja ambapo mgonjwa alikuwa analazimika kupasuliwa paja ili kupata
mishipa yake iliyokuwa inatumika katika kufanya matibabu hayo ya moyo.
Ajabu la pili kutokana na upasuaji huo mpya na wa aina yake; ni lile
la mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji huo wa kuzibua mishipa ya moyo bila
kufungua kifua kuruhusiwa kurudi nyumbani baada ya saa nne tangu
afanyiwe upasuaji.
Hatua hiyo ni tofauti na upasuaji wa awali wa kutumia mshipa wa paja
ambapo mgonjwa alikuwa analazimika kukaa hospitali kwa zaidi ya saa 24
ili kuangalia maendeleo ya afya yake.
Ajabu la tatu katika matibabu hayo ni hatua ya wageni hao kutoka
Taasisi ya IIRO kujifunza vitu vingi na kupata uzoefu mpya wa baadhi ya
magonjwa na mambo ya kiteknolojia katika Taasisi ya JKCI ambayo katika
nchi yao hakuna.
Mufti awafumbua macho
Watanzania Akizungumzia matibabu hayo ya aina yake jana; Shehe Mkuu
wa Tanzania; Mufti Abubakar Zubeir aliwaasa Watanzania kupata matibabu
hasa ya magonjwa ya moyo hapa nchini ili kuepuka gharama za kwenda
kupata matibabu nje ya nchi ambako gharama yake ni kubwa.
Shehe Zubeir alitoa mwito huo katika hafla ya kuwaaga madaktari hao
bingwa wa IIRO wa Saudi Arabia waliofika nchini kushirikiana na wenzao
wa JKCI katika upasuaji huo. “Kazi iliyofanywa hapa ni kuhakikisha watu
wanapata tiba nzuri, watu wasiende nje ya nchi kutibiwa kwani gharama
yake kwa mtu mmoja ni zaidi ya shilingi milioni 30, niwashitue
Watanzania kuwa tiba hizi zinapatikana hapa kwenye taasisi hii ya JKCI,”
alisema.
Alisema gharama ambayo mgonjwa atakwenda kutibiwa nje ya nchi ni
kubwa ambapo si watu wengi wanaweza kuimudu ndiyo maana serikali pamoja
na taasisi nyingine wameomba kambi hizo za matibabu kuja nchini kufanya
matibabu na pia kutoa ujuzi wa madaktari waliopo.
Mkurugenzi JKCI ahimiza upimaji wa afya
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya JKCI, Profesa Mohamed Janabi
alisema kambi hiyo ya madaktari kutoka Saudi Arabia ilienda sambamba na
kutoa mafunzo kwa madaktari wa JKCI na pia kubadilishana ujuzi kitu
ambacho kimewajengea uwezo.
“Faida ya upasuaji wa aina hii ni kumuwezesha mgonjwa kutoka chumba
cha upasuaji akiwa anatembea mwenyewe na baada ya saa nane anaweza
kuruhusiwa kutoka hospitali kama anaendelea vizuri, kwa hiyo kambi hii
ni faida sana kwetu,” alisema Profesa Janabi.
Aidha aliwasisitiza wananchi kupima afya zao mara kwa mara jambo
ambalo litawasaidia kujua kama wana matatizo ya moyo hivyo kupata tiba
kwa wakati. “Changamoto kubwa tunayokutana nayo ni kuwa wagonjwa wengi
tunaowapokea ni mioyo yao kuwa katika hali mbaya.”
Aliishukuru taasisi ya IIRO kwa kutuma wataalamu hao kuja kutoa
huduma ya matibabu ambayo iliambatana na mafunzo kwa madaktari wa
taasisi ya JKCI.
Balozi, Wizara wasifu ushirikiano
Balozi wa Saudi Arabia nchini, Mohammed bin Mansour Almalik alisema
kuja kwa madaktari hao ni ishara kwamba Tanzania na Saudi Arabia wana
ushirikiano mzuri, alisema ushirikiano huo hautaishia kwenye sekta ya
afya pekee bali pia katika sekta nyingine.
Mwakilishi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Dk Dorothy Gwajima alisema wizara hiyo itaendeleza ushirikiano
wa aina hiyo na taasisi mbalimbali ili wataalamu wa ndani katika sekta
ya afya wapate ujuzi wa kutosha na pia kujifunza teknolojia mpya kuepuka
gharama za kumpeleka mgonjwa kutibiwa nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment